Mohammad Marandi, mtaalam na mshauri wa vyombo vya habari wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia huko Vienna, ameandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba: "Kama Iran ingekuwa inafuatilia silaha za nyuklia, ingetengeneza silaha hizo mwaka mmoja uliopita."
Marandi ameongeza kuwa: Wakati wa mazungumzo ya nyuklia huko Vienna, tawala za Magharibi zilidai kuwa mradi wa nyuklia wa Iran "unafikia hatua ya kutorudi nyuma tena"; hii ni pamoja na kuwa mazungumzo ya kuiondolea Iran vikwazo na kurejea Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA yamesitishwa kwa miezi kadhaa kutokana na tabia ya Marekani ya kutaka kudhibiti kila kitu na kutojali uhalisia wa mambo, na vilevile uvurugaji wa nchi za Ulaya. Amesisitiza kuwa, viongozi wa Iran wametangaza mara kwa mara kwamba Tehran iko tayari kuanza tena mazungumzo na kuyafikisha kwenye hitimisho.
Wakati huo huo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameashiria mazungumzo yake ya hivi karibuni na Josep Borrell, Mkuu wa Zera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya huko Baghdad nchini Iraq na kusema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuchukua hatua za mwisho za kufikia makubaliano ya nyuklia na kufuta vikwazo vya kidhalimu."
Hata hivyo Hossein Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa: "Dirisha la kufikia makubaliano la Iran halitakuwa wazi milele."
342/